Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions

Name

Margaret Simwanza Sitta

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Urambo

Primary Question

MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:- Je, lini Serikali itajenga jengo jipya la Mahakama ya Mwanzo Urambo kutokana na hali mbaya ya jengo lililopo sasa hasa kipindi cha mvua?

Supplementary Question 1

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaipongeza Serikali kwa majibu mazuri yaliyotolewa hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hali ya Mahakama ya Mwanzo Wilayani Urambo ni mbaya sana, kwanza ni kutokana na kujengwa wakati wa mkoloni, majengo yale au jengo lile limeezekwa kwa asbestos, sasa si rahisi sasa hivi kukuta majengo yaliyoezekwa kwa asbestos kwa sababu ni material iliyokuwa inatumika enzi za ukoloni zile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ni mbaya na hasa kipindi cha mvua jengo zima huwa linazungukwa na maji na nilishachukua picha zake kiasi ambacho wafanyakazi ndani ya jengo lile la Mahakama ya Mwanzo, wanapata shida hata kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali iko tayari na hasa Mheshimiwa aliyesimama na kujibu maswali, anaweza kupata nafasi ya kuja kujionea mwenyewe hali ngumu iliyoko katika Mahakama ya Mwanzo Wilayani Urambo?

Name

Zainab Athuman Katimba

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Answer

NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwanza kumpongeza Mheshimiwa Margaret Sitta kwa swali lake zuri, kwa sababu lengo hapa anataka kuona upatikanaji wa haki katika Jimbo lake unaendelea kuimarika kwa kuwa na miundombinu bora ya Mahakama ya Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhahiri kabisa Serikali ya Awamu ya Sita imefanya uwekezaji mkubwa kabisa wa kipekee na wa kimageuzi wa jumla ya shilingi bilioni 524.9 katika kipindi hiki tu cha miaka mitano, kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii ya mahakama. Pia kufanya mapinduzi makubwa ya matumizi ya TEHAMA katika Muhimili wa Mahakama kwa ajili ya kuboresha huduma hizi za upatikanaji wa haki, kwa hakika hii ni legacy ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Margaret Sitta, kwamba katika mkakati huu, katika huu mpango wa ujenzi na ukarabati wa majengo ya Mahakama, lengo ni kufika katika maeneo mbalimbali ya nchi, kuboresha miundombinu ya Mahakama ikiwemo Mahakama za Mwanzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie, kama nilivyojibu katika jibu la msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2027/2028, jengo la Mahakama hii ya Mwanzo litajengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nipo tayari nikitoka hapa tutakaa na yeye, tutazungumza, tutapanga ratiba ili niweze kufika kama alivyotaka yeye Mheshimiwa Mbunge, kwenda kujionea hali halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali na Muhimili wa Mahakama unafahamu uhitaji, ndiyo maana tayari unaendelea kufikia maeneo mbalimbali kwa awamu kwa ajili ya kuhakikisha kwamba miundombinu hii ya mahakama inajengwa kwenye maeneo ambayo yanahitaji ujenzi na inakarabatiwa kwenye maeneo ambayo ni chakavu. Kwa hiyo, kwa awamu tutakuja kufika pia katika Mahakama hii ya Mwanzo ya Urambo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inajengwa na inakuwa na ubora ambao utaboresha upatikanaji wa haki kwa wananchi. Ahsante.